
KUTANGAZWA MWENYEHERI MPYA KUTOKA CONGO
Maelezo Zaidi
*KUTANGAZWA _'MWENYEHERI'_ MPYA KUTOKA CONGO.* Floribert Bwana Chui Bin Kositi kutoka CONGO atatangazwa kuwa MWENYEHERI tarehe 15 Juni 2025. Mlei wa Kongo Floribert Bwana Chui, anayetambuliwa kuwa "Shahidi wa uaminifu na uadilifu wa kimaadili," atatangazwa kuwa mwenye mwenye heri siku ya Jumapili, tarehe 15 Juni 2025, huko Roma, kwenye Kanisa Kuu la 'Mtakatifu Paulo, katika adhimisho la Sherehe ya Utatu Mtakatifu. Katika kutangaza tukio hili la furaha, Askofu Willy Ngumbi M. Afr, Askofu wa jimbo Katoliki Goma - DRC, alifafanua kwamba eneo na tarehe husika za kutangazwa kwake ziliwasilishwa kwake na Dicastery a inayohusika (Dicastery for the Causes of Saints). Kifo cha mtumishi wa Mungu Floribert Bwana Chui Bin Kositi, aliyekuwa muumini mlei mwaminifu kutoka Jamhuri ya Kongo, aliyefariki akiwa na umri wa miaka 26 mwaka 2007, kilitambuliwa na Hayati Papa Francisko tarehe 25 Novemba 2024. Hayati Papa Francis aliidhinisha kuchapishwa kwa agizo hilo la kutangazwa mwenye heri. Tarehe 20 Aprili 2025, Jumapili ya Pasaka, Askofu wa Goma alitoa Taarifa ya Kichungaji kwa waamini Wakristo na wote wenye mapenzi mema, akitangaza na kuwajulisha furaha ya kutangazwa Mwenyeheri, mlei huyu kijana, aliyeelezewa kama kielelezo cha “uaminifu na uadilifu wa kimaadili.” "Furaha hii sasa imethibitishwa kwa vile Dicastery imetaja mahali na tarehe ya tukio hilo. Hakika ni Jumapili, tarehe 15 Juni 2025, huko Roma, katika adhimisho la Sherehe ya Utatu Mtakatifu," aliandika Askofu Ngumbi. Katika Taarifa yake, askofu wa Kongo anakumbuka historia ya Floribert Bwana Chui kama "mlei kijana aliyezaliwa tarehe 13 Juni 1981, huko Goma, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na kuuawa huko huko Goma mnamo 8 Julai 2007," kwa sababu ya chuki ya kidini. Akiwa anatoka katika familia tajiri, Floribert alisoma sheria na uchumi. Alikuwa Mfanyakazi mwaminifu aliyeishi Injili kwa maneno na matendo. Kijana huyu wa Kikongo alianza maisha yake ya kitaaluma huko Kinshasa kama Afisa wa forodha katika Ofisi ya Udhibiti ya Kongo (OCC), wakala unaohusika na udhibiti wa forodha na bidhaa. Alihusika katika kutathmini bidhaa zinazovuka mpaka wa mashariki wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Baadaye, alihamishwa hadi jiji la Goma kama mkuu wa ofisi ya OCC. Wakati wa masomo yake, Floribert Bwana Chui alijiunga na Jumuiya ya Sant’Egidio, akajitolea sana katika kusaidia watoto yatima na wa mitaani. Katika kutekeleza majukumu yake, Floribert alikabiliwa na tatizo la kimaadili: kuruhusu kuingia DRC chakula kisichofaa kilichoagizwa kutoka nchi jirani ya Rwanda. Chakula kilichoagizwa hakikuwa na nyaraka na idhini sahihi ya kuuzwa na uthibitisho wa kufaa kwa matumizi ya binadamu nchini DRC. Kulingana na ushuhuda, "Bwana Chui alichagua kufa kuliko kuruhusu au kupitisha chakula hicho ambacho kingeweza kuwadhuru watu wengi ambao wangekitumka." KIFO CHA FLORIBERT BWANA CHUI. Kukataa kwake fedha chafu (hongo/rushwa) zilizohusishwa na uingizaji haramu wa bidhaa za chakula chenye sumu ilikuwa sababu iliyopelekea kifo chake. Floribert aliona na kuamini wazi kuwa ni kinyume kabisa cha maadili kukubali kuhongwa kwa dola kadhaa na kupitisha bidhaa zenye sumu zinazokusudiwa kutumiwa na watu. Badala yake, Floribert aliamuru kuharibiwa kwa viroba vya mchele vilivyokwisha muda wake na kukataa kupokea rushwa ile. Uadilifu wake huu aliouonyesha katika kazi yake ulisababisha kutekwa nyara na hatimaye kuuawa. Mashuhuda waliomfahamu na kuwahi kufanya naye kazi walibainisha zaidi kwamba Floribert alisema mara nyingi: “Pesa zitakwisha haraka. Lakini vipi kuhusu wale ambao watatumia bidhaa hizi? Je, ninaishi kwa ajili ya Kristo au sivyo? Ndiyo maana siwezi kukubali. Ni bora kufa kuliko kukubali pesa hizi.” Akiwa na umri wa miaka 25, Floribert Bwana Chui alitekwa nyara na kuuawa usiku wa tarehe 7/8 Julai 2007 huko Goma kwa kukataa kukubali rushwa na kuzima mpango wa kuvusha bidhaa za vyakula ambavyo havikuwa vinafaa kwa matumizi ya binadamu. Askofu Faustin Ngabu wa Goma alisema, "Floribert Bwana Chui Bin Kositi alikufa kwasababu ya kuwa mkweli na mwaminifu kwa imani yake ya Kikristo. Alikuwa mtu ambaye alionyesha ushupavu na uhuru wake katika hali ngumu sana. Alichokipata kilikuwa dhihirisho la nguvu la imani yake ya Kikristo." Kufuatia Misa ya kutangazwa mwenye heri huko Roma, Misa ya shukrani itafanyika huko Goma siku ya Jumanne, tarehe 8 Julai, siku ya kumbukumbu ya kifo chake kilichotokea tarehe kama hiyo mwaka 2007. Askofu Ngumbi anasema kwamba, kutangazwa kwa muumini huyu kuwa Mwenyeheri ni chanzo cha matumaini na sababu ya kumshukuru Bwana anayeendelea kudhihirisha maajabu yake. Askofu pia alisisitiza kwamba kifo cha kishahidi cha Floribert ni heshima kwa Kanisa la Kongo na Jimbo la Goma, na hivyo akatoa wito kwa kila mtu kuzidi kujitolea zaidi katika kutenda haki, amani na kudumisha undugu katika imani na kumtumaini Kristo Mfufuka. Floribert Bwana Chui atakuwa Mkongo wa nne kutambuliwa na kutangazwa kuwa mwenyeheri, baada ya kutangazwa kwa Mwenyeheri Anuarite Nengapeta, Mwenyeheri Isidore Bakanja, na Mwenyeheri Padre Albert Joubert, ambaye alitangazwa mwenye heri pamoja na wamisionari watatu wa Xaverian tarehe 18 Agosti 2024 huko Uvira, Mashariki mwa DRC. Utukufu kwa Mungu juu Mbinguni, na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia. Damu ya mashahidi ni mbegu ya imani. Tumsifu Yesu Kristu.
