
Kongamano la vijana Roma Mwaka 2025 Mahujaji wa matumaini
Maelezo Zaidi
Baba Mtakatifu Leo XIV, Jumamosi tarehe 2 Agosti 2025 amewaongoza vijana zaidi ya milioni moja kufanya mkesha kwenye uwanja wa Tor Vergata, mjini Roma, kama sehemu ya maadhimisho ya Kufunga Jubilei ya Vijana kwa Mwaka 2025. Katika majadiliano yake na vijana wa kizazi kipya, Baba Mtakatifu Leo XIV amegusia pamoja na mambo mengine kuhusu: Urafiki wa kijamii; Ujasiri wa kuamua na kuchagua na hasa zaidi katika kufuata wito wa: maisha ya ndoa na familia, upadre pamoja na maisha ya kuwekwa wakfu. Amewataka vijana kujikita katika kufuata mambo mazuri kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kumwilisha Injili ya huduma ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Vijana wajitahidi kuboresha maisha yao kwa njia ya: Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa, Maisha ya Sala sanjari na Ibada ya Kuabudu Ekarisri Takatifu. Kwa hakika vijana wanaweza kukutana na Kristo Yesu katika hija ya maisha yao kwa njia ya Kanisa. Amewataka vijana kuwa ni vyombo na mashuhuda wa imani, furaha na ujasiri tayari kujikita katika ujenzi wa dunia inayosimikwa katika msingi wa utu, heshima na haki msingi za binadamu; watafute na kuambata ukweli kwa ari na moyo mkuu; wajenge urafiki wa kijamii unaoweza kuwa ni njia muafaka ya ujenzi wa amani Baba Mtakatifu Leo XIV Dominika tarehe 3 Agosti 2025 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kufunga maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo kwa vijana na kuhudhuriwa na: Vijana zaidi ya milioni moja kutoka katika nchi 146; Mapadre elfu saba na Maaskofu ni 450, na wadau wa tasnia ya mawasiliano walikuwa ni 850, matendo makuu ya Mungu. Baba Mtakatifu Leo XIV amewakumbusha kwamba, Ekaristi Takatifu ni Sakramenti na ni sadaka ya upendo kutoka kwa Kristo Yesu kwa ajili ya waja wake, mwaliko kwa vijana kufuata ile hija ya Wanafunzi wa Emau waliobahatika kuandamana na Kristo Yesu katika safari yao ya matumaini bila kumtambua, kwani macho yao yalikuwa yamefumbwa! Wakampokea na kumkaribisha kama mwandani wa safari ya maisha yao. Walikuwa wakisafiri kwa huzuni kubwa na hali ya kukata tamaa kwa sababu ya kifo cha kikatili kilichomkuta Kristo Yesu. Walikuwa wakimtumainia kwamba Yeye ndiye Masiha na Mkombozi wao. Wanafunzi wa Emau walikuwa na majonzi makubwa mioyoni mwao kwani Fumbo la Msalaba, yaani mateso na kifo cha Kristo Yesu liliwaachia machungu makubwa kwani liliyeyusha matumaini na maisha yao; wakaonekana kushindwa vita hata kabla ya kuianza. Lakini, wakamtambua Kristo Yesu wakati wa kuumega mkate na hapo hapo akatoweka tena machoni pao! Nao wakaambiana, Je, mioyo yetu haikuwaka ndani yetu pale alipokuwa akizungumza na kufafanua Maandiko Matakatifu? Rej Lk 24:13-35
